MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA WANAWAKE, TABORA.
Thursday, March 8, 2018

Tarehe 08 Machi, 2018

Na Daudi Nasib, Katibu Mtendaji

Sherehe za maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Mkoa wa Tabora zilikuwa za aina yake mwaka huu. Mgeni rasmi alikuwa si mwingine bali Mheshimiwa Mama Salma Kikwete (MB), mkkwe wa Rais Mstaafu na Mwenyekiti wa WAMA. Mama Kikwete anafahamika kuwa ni mtetezi mahiri wa Maendeleo ya wanawake na wasichana Tanzania na duniani kote. Hivyo haikuwa ajabi kwa uongozi wa Mkoa wa Tabora kumualika ili kuzipamba sherehe hizo wala kwake kuukubali mwaliko huo.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na mamia ya wanawake kutoka kada  mbalimbali wakiwemo watumishi wa uma, wajasiriamali,  wanafunzi wa vyuo na maeneo mengine. Kama kawaida walivalia sare zao maridadi za vitenge vilivyoifanya madhari ya sherehe kupendeza sana na kubwa zaidi kuonesha mshikamano mkubwa miongoni mwa wanawake wa Tabora pamoja na wanaume wanaojali wakiongozwa na Mheshimiwa Agrey Mwanri, Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

 

Katika hotuba yake, Mheshimiwa Mama Salma Kikwete alitoa lshukrani zake kwa uongozi wa Mkoa wa Tabora na kwa waandaaji wa sherehe hizi kwa kumualika na kwa mapokezi mazuri na ukarimu waliomuonesha. Hali kadhalika, alitoa pongezi nyingi kwa wana-Tabora, kwa kuwa na utaratibu mzuri wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake kwa uzito unaoistahili siku hiyo adhimu na muhimu kwa Wanawake na hata kwa Wanaume pia. Halikadhalika alitoa kongole tele kwa CG FM Radio ambao wamekuwa wanaratibu maadhimisho hayo kila mwaka kuanzia 2004. Ni jambo jema linastohakili kutambuliwa na kupongezwa na wote. Aliwataka waendelee na moyo huo wa upendo kwa akina mama.

Heshimiwa Mama Kikwete alifurahishwa sana na kauli mbiu ya kitaifa ya siku ta Kimataifa ya Wanawake isemayo: ‘Kuelekea Uchumi wa Viwanda. Tuimarishe usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake Vijijini”. Kwa namna fulani inashabihiana na historia ya kuwepo kwa siku hii. Aliwakumbusha washiriki kwamba, chimbuko la siku ya wanawake duniani ni kitendo cha ukatili na udhalimu mkubwa walichofanyiwa wanawake katika kiwanda kimoja cha nguo jijini New York Marekani tarehe 08 Machi, 1857. Katika kiwanda hicho kulitokea mgomo wa wafanyakazi kupinga mazingira mabaya ya kazi. Uongozi wa kiwanda hicho uliamua kuwafungia wafanyakazi wanawake katika jengo moja na kuliteketeza kwa moto. Inakadiriwa kuwa takribani wanawake 129 walipoteza maisha. 

Alieleza kwamba mafanikio makubwa yamepatikana katika Nyanja zote, hata hivyo akatoa tahadhari kwani Juhudi kubwa bado zinahitajika. Sote tunafahamu kwamba mzigo mkubwa wa umasikini katika jamii zetu huwaelemea wanawake zaidi kuliko wanaume. Tunafahamu, vile vile, kwamba madhara ya huduma duni za afya humlemea mwanamke zaidi kuliko mwanamume. Alito takwimu za kitaifa zinazoelezea changamoto katika maeneo ya Elimu, Afya, uchumi na unyanyasaji wa ki-jinsia.

Kwa upande wa elimu alieleza kwamba katika nchi yetu asilimia 15 ya Wanawake hawajawahi kwenda shule ukilinganisha na asilimia 8 ya wanaume. Hivyo alisisitiza uwekezaji katika eneo la elimu ili kutoa suluhisho la kudumu kwa changamoto za wanawake. Alielezea changamoro ya mimba za utotoni ambazo kwa mkoa wa Tabora ni kubwa zaidi. Mkoa wa Tabora unashika nafasi ya Pili kitaifa kwa kuchangia asilimia 43 ya matukio ya watoto kupata ujauzito katika umri mdogo. Mkoa wa Katavi ndio unaongoza nchini ambapo ni asilimia 45. Tabora iko juu ya wastani wa Taifa ambao ni asilimia 27, ambao pia ni mkubwa mno.

Kwa upande wa uchumi Mheshimiwa mama Kikwete alieleza kwamba ni asilimia 48 tu ya wanawake ndiyo wanaofanya kazi za kulipwa fedha ukilinganisha na asilimia 76 ya wanaume. Wanawake wengi zaidi asilimia 22 hujishughulisha na ajira zisizo na ujuzi ukilinganisha na wanaume asilimia 11.Ni wanawake wachache tu asilimia 4 wanaofanya shughuli zenye ujuzi (manual skilled labour) ukilinganisha na wanaume asilimia 18. Hali hii husababisha tofauti kubwa ya kipato baina ya wanawake na wanaume. Vile vile ina athari kubwa kwenye nafasi ya mwanamke katika maamuzi yanayoihusu familia na wakati mwingine hata yanayomhusu yeye mwenyewe. Tunaarifiwa kwamba wanawake wachache sana kama asilimia 46 tu ndio hushiriki katika maamuzi yanayohusu manunuzi katika familia zao. Na kwa bahati mbaya takriban asilimia 20 ya wanawake hawashiriki kabisa maamuzi yoyote katika kaya. Wakati mwingine hata uamuzi wa kwenda kuwasabahi ndugu zao lazima yafanywe na mume. Mambo haya humfanya mwanamke kujisikia kuwa mtu dhalili na kutokujiamini.Unyonge huu nao hatuna budi kuupiga vita, alisema Mama Kikwete.

Terms of Use | Privacy Policy | SitemapCopyright © 2010 - 2018 WAMA Foundation, All Rights Reserved